Teuvo Kopra:

 

Mambo yatakayotokea katika hukumu ya mwisho

 

 

Tusome Biblia.

 

43. Basi hawa ndio wafalme waliomiliki katika nchi ya Edomu, kabla hajamiliki mfalme awaye yote juu ya wana wa Israeli; Bela, mwana wa Beori; na jina la mji wake ni Dinhaba. 44. Bela akafa, naye Yobabu, mwana wa Zera, wa Bosra, akamiliki badala yake. 45. Yobabu akafa, naye Hushamu, wa nchi ya Watemani, akamiliki badala yake. 46. Hushamu akafa, naye Hadadi, mwana wa Bedadi, akamiliki badala yake, ambaye aliwapiga Midiani katika uwanja wa Moabu; na jina la mji wake ni Avithi. 47. Hadadi akafa, naye Samla, wa Masreka, akamiliki badala yake. 48. Samla akafa, naye Shauli, wa Rehobothi karibu na Mto, akamiliki badala yake. 49. Shauli akafa, naye Baal-Hanani, mwana wa Akbori, akamiliki badala yake. (1NYA 1:43-49)

 

Haya yalitokea miaka elfu tatu, au elfu nne iliyopita. Hapa tunaelezwa juu ya wafalme. Wao walizaliwa, walikua, na wakawa wafalme. Walitawala miaka kadhaa, baadaye walizeeka wakafa. Tena akaja mfalme mpya aliyetawala, akazeeka akafa.

 

Maisha ya mwanadamu ndivyo yalivyo. Mwanadamu anazaliwa, anaishi baadaye anafariki. Tena mtu  mwingine anazaliwa, anaishi na hatimaye anakufa. Kizazi kingine kinatokea.

 

Hapa kulikuwa na mlolongo wa watu, au kama mnyororo wa watu. Walizaliwa na wakaanza kuishi kuelekea siku ile watakapokufa. Babu zetu walikuwa katika mlolongo huo. Hao nao  walifariki na kizazi kingine kikazaliwa. Lakini kila mwanadamu aliyezaliwa ni lazima atakufa.

 

Hata sisi tulizaliwa tumeingia kwenye mstari wa wale wanaoelekea mautini. Siku moja tulizaliwa hapa duniani, tunaishi hadi sasa, lakini siku moja maisha yetu yatakoma. Baada ya kifo tutaingia katika umilele, kutoka huko hakuna kurudia tena haya maisha ya duniani, kama haya tunayoishi sasa. Tumepewa maisha haya mafupi, ili wakati wa uhai wetu tuweze kumtafuta Mungu.

 

23. Kwa imani Musa, alipozaliwa, akafichwa miezi mitatu na wazazi wake, kwa sababu waliona kwamba ni mtoto mzuri; wala hawakuiogopa amri ya mfalme. 24. Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; 25. akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; 26. akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo. 27. Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana. (EBR 11:23-27)

 

Tumesoma katika mstari wa ishirini na sita: ... akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.

 

Musa aligeuza macho yake akaangalia umilele. Yeye alijua kwamba, anaishi muda mfupi tu hapa duniani na baadaye ataanza umilele usiokuwa na mwisho. Hiyo ilitegemea na uchaguzi wa maisha yake.

 

Je, unapenda kujua kilicho mbele yetu katika umilele? Mimi ninapenda kujua kwani nitakaa huko milele.

 

Sasa tuangalie kidogo kuhusu wakati wa umilele, yaani baada ya maisha haya.

 

Tunajua wote ni lazima tufe. Wakati wa kurudi kwa Yesu tutabadilishwa, mabadiliko haya yanaweza kulinganishwa na mauti.

 

12. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. 13. Bahari ikawatoa wafu walikuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. 14. Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. 15. Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto. (UFU 20:12-15)

 

Sehemu hii inaeleza juu ya hukumu ya mwisho. Baada ya kifo watu watagawanywa katika makundi mawili. Waliookoka wataingia Paradiso baada ya kifo chao. Kuhusu Paradiso Biblia inatumia majina:

- Mbingu ya tatu (2KOR 12:2,4).

- Kifua cha Ibrahimu (LK 16:22).

- Peponi (2KOR 12:4).

 

Biblia inatumia jina Peponi, lakini watu wengi wanatumia jina: Paradiso. Peponi, Kifua cha Ibrahimu, Mbingu ya tatu na Paradiso ni sawa sawa.

 

Wapagani, au wale ambao hawajazaliwa mara ya pili wataenda Kuzimu. (AYU 24:19, LK 16:23).  Zote hizi ni nyumba za kusubiri umilele. Biblia inaeleza kuhusu nyumba hizi, kwamba kuzimu ni mahali pabaya, mahali pa kutisha sana. Huko kuna kilio, huzuni na mateso.

 

Biblia inaeleza kwamba Paradiso ni mahali pazuri sana. Wakati mambo yote ya nyakati za mwisho, unapokaribia, ndipo wakati wa hukumu ya kiti cheupe cha enzi utakuwa umefika. Hayo tumesoma katika Ufunuo. Sisi sote tutakuwepo mbele ya kiti hicho cheupe cha hukumu. Hapo watakuwepo wale waliokuwa wanasema kwamba hakuna Mungu, hakuna Mbingu wala Jehanamu. Hata wao ni lazima watakuwepo huko. Huko watakuwepo hata Waislamu ambao hawamwamini Yesu kuwa Mungu. Wote wanaomfuata Yesu watakuwa huko. Walio watesa Wakristo watakuwepo huko. Walio abudu roho chafu watakuwepo.

 

Kwanza watu watagawanywa makundi mawili. Katika kundi la kwanza, watakuwepo wale ambao majina yao yameandikwa kwenye kitabu cha uzima wakati ule walipookoka. Kundi la pili ni wale watu ambao majina yao hayamo katika kitabu cha Uzima. Wakati ule ulipookoka jina lako liliandikwa katika kitabu cha Uzima. Labda leo jina lako limeandikwa katika kitabu cha Uzima. Liliandikwa wakati ule malaika wakishangilia kuokoka kwa mtu mmoja. Labda wakati wa safari yako ulikuwa unajikwaa, lakini jina lako liko ndani ya kitabu hicho kwa sababu hukuacha wokovu.

 

Tumesoma kwamba  ...wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya .. kiti cha enzi. Wakubwa ni akina nani? Maisha ya wokovu yanaamua. Wadogo ni wale wasiofundisha Neno la Mungu kwa usahihi. (Mt 5:19)

 

Kwa ufupi twende mbele ya kiti cha enzi cha makundi haya mawili. Tuangalie kidogo jinsi gani watu watakavyohukumiwa. Kwanza tuwatembelee waliotoka Kuzimu na tusikilize maneno ya hakimu.

 

Waliotoka Kuzimu yaani wale waliokufa bila ya wokovu, bila ya kumwamini Yesu. Mtu mmoja atatoka huko. Kama leo yupo mtu yeyote hapa ibadani ambaye hajaokoka, na wala hataki kuokoka. Baada ya kufa atakwenda Kuzimu na dhambi zake. Labda ni wewe, au mwingine atafika mbele ya hakimu. Hakimu atafungua kitabu ambacho kina matendo ya watu. Kitabu hicho tunaweza kukiita: Kitabu cha Matendo. Kitabu cha Uzima ni kile kilicho na majina ya wale waliomwamini Yesu.

 

Mtu fulani anapokuja kitabu cha Matendo kinafunguliwa. Labda huyo mtu ni wewe, ambaye hutaki kuokoka. Labda humu kuna matendo mengi mazuri katika kitabu cha Matendo. Labda yeye alipenda mambo ya kidini kama mikutano, maombi, na alisoma Biblia. Labda amefanya matendo mazuri na aliwasaidia watu. Yeye angeweza kuwa na hazina nyingi zinazomsubiri mbinguni.

 

Lakini yeye hajazaliwa mara ya pili. Yeye hajaokoka, yaani hajamwamini  Yesu Kristo. Yeye hajaanza kamwe kumfuata Yesu katika njia ya mbinguni. Labda atajitetea mbele ya hakimu kwa kusema: "Mimi nilifanya mambo mazuri. Hata niliomba mara nyingi. Hata nilishiriki meza ya Bwana katika kanisa fulani na kuimba nyimbo za kidini. Je, hayo hayatoshi? Je, si ninaweza kuingia mbinguni kwa matendo hayo?"

 

Ndipo hakimu atasema: "Tusome Injili ya Yohana, sura ya tatu, na mstari wa tatu." Na hakimu atasoma: Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.  (YN 3:3)

 

Na hakimu anaendelea kusema: "Ingawa ulitenda matendo mazuri, lakini hujazaliwa mara ya pili, yaani hujaokoka. Hivyo ufalme wa Mungu si wako!" Nafikiri huyu mtu atakosa neno la kusema.

 

Biblia ni kitabu cha sheria kwa wasiookoka siku ya hukumu ya mwisho. Wasiookoka watahukumiwa kadiri ya sheria ya Biblia. Hata kosa dogo tu linatosha kuhukumiwa. Mtu huyu hatapokea malipo mbinguni, kulingana na matendo yake mazuri. Yeye atagundulika kuwa ni mwenye hatia kwa sababu damu ya Yesu haijasafisha dhambi zake. Dhambi zinasafishwa wakati wa kuokoka, yaani wakati wa kuzaliwa mara ya pili na baada ya hapo damu ya Yesu inatupa uthamani wa mbinguni iwapo tunatunza wokovu. Asiyeokoka, atahukumiwa kulingana na matendo yake yote. Labda watu kama hawa watakuwa wengi mbele ya kiti cha enzi cha hukumu.

 

Sasa tuangalie ni jinsi gani mtu, aliyeokoka atakavyokaribia kiti cha hakimu. Labda huyo ni wewe. Wewe utasimama mbele ya hakimu. Kwanza hakimu ataangalia kama jina lako limo katika kitabu cha Uzima. "Ndio - limo!" hakimu atasema. Hakimu atasema: "Liliandikwa humo siku ile ulipookoka." Labda leo, au zamani. Na limekuwepo huko ingawa imani yako ilikuwa dhaifu.

 

Halafu kitabu cha matendo kitafunguliwa. Labda utaogopa kidogo ukikumbuka maisha yako yalivyokuwa dhaifu. Wewe ulipotoka mara nyingi na hata ulitenda dhambi, lakini pia ulitubu. Sasa unafikiri kwamba wakati wa hukumu ya mwisho hayo yote yatasomwa kutoka katika kitabu cha Mungu ambako matendo ya watu yameandikwa.

 

Hakimu atafungua kitabu, lakini atakuta matendo mazuri tu. Hakimu atasema: "Hakuna matendo mabaya kwani yote yamefutwa". Labda wewe utasema: "Nilianguka na kukosea mara nyingi! Nilikuwa msafiri mnyonge katika njia ya kwenda mbinguni." Ndipo hakimu atasema: "Hiyo si kweli. Wewe si msafiri dhaifu wala hujatenda dhambi vitabu vyetu vinaonyesha hivi!" Lakini wewe utabisha: "Mimi ninayakumbuka vizuri makosa yangu. Hata wengine pia wanakumbuka jinsi gani nilivyoanguka mara nyingi katika njia ya kwenda Mbinguni." Ndipo Hakimu atakujibu: "Hujawa nazo! Vitabu vyetu vinaonyesha kwamba hujawa na dhambi wala udhaifu. Hapa watu wanahukumiwa kulingana na vitabu vyetu na si kulingana na mawazo yako."

 

Na labda Hakimu atakukumbusha kuhusu mambo machache, yale yaliyosemwa hapa duniani mara nyingi. Atakueleza juu ya kazi ya Yesu ya upatanisho. Yesu alienda msalabani kwa ajili yako. Wewe ulifanya dhambi, sio Yesu lakini dhambi zako ziliwekwa juu ya Yesu, na yeye aliadhibiwa kwa ajili ya dhambi zako.

 

Hivyo adhabu hiyo imekwisha pitishwa. Damu ya Yesu ilichuruzika msalabani, damu yake imefuta dhambi zako kutoka katika vitabu vya Mungu. Hakimu ataendelea: "Ndio maana hakuna dhambi humo wala hukufanya matendo yoyote mabaya katika maisha yako kwa sababu damu ya Yesu ilizifuta zote. Kwa hiyo hazimo”.

 

“Matendo yako mazuri yatapatikana humo kitabuni:

- Uliwasaidia majirani.

- Uliwatia moyo na kuwafariji waliokuwa katika matatizo.

- Uliwapa maskini chakula

- Ulitumika kanisani.

- Ulitoa sadaka kwa ajili ya kazi ya kanisa.

- Na mengine mengi.

Hayo yote yameandikwa vizuri kwenye kitabu. Hata mambo uliyosahau yameandikwa”.

 

Halafu Hakimu atasema kwamba, kwa haya yote unapokea thawabu kubwa, lakini haya hayakuwezeshi kuingia Mbinguni. Ili kuingia Mbinguni unahitaji wokovu na kuenenda katika wokovu. Damu ya Yesu inawaweka waliookoka kuwa na uthamani wa Mbinguni.

 

Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.  (RUM 8:1)

 

Mwenendo wetu mbaya unaleta huzuni kwa Yesu, watu wengine, na kwetu pia. Unachelewesha  safari yetu, na kuifanya kuwa ngumu, lakini hautuzuii kuingia Mbinguni. Lakini mtu akiacha wokovu na kuchagua dhambi, wokovu wake haukumbukwi. Ukifanya dhambi kuna hatari kubwa ya kupoteza imani yako. Wakati huo damu ya Yesu haitakufanya kuwa msafi. Na baadaye utahukumiwa kadiri ya matendo yako na hukumu ni hukumu ya milele.

 

Sasa tumechunguza kuhusu watu wawili mbele ya kiti cheupe cha enzi. Mmoja jina lake halikuwepo katika kitabu cha uzima lakini mwingine lilikuwepo.

 

Tumesoma katika Ufunuo sura ya ishirini, mstari wa kumi na tano, kwamba: Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto. (UFU 20:15)

 

Mtu fulani anaweza kufikiri labda wakati mrefu, utapita kwa kutengeneza mambo ya kila mmoja na matendo ya watu wote. Ndivyo itakavyokuwa, lakini katika umilele kutakuwa na muda wa kutosha. Hata ipite miaka milioni, katika umilele kuna muda wa kutosha.

 

Kabla ya wale ambao majina yao hayamo katika kitabu cha uzima kuingia upotevuni, na wale ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima kuingia Mbinguni, kitatokea kitu fulani. Na baada ya kutokea kitu hicho, wale ambao majina yao hayamo katika kitabu cha uzima watakwenda Jehanamu, na wale ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima watakwenda Mbinguni.

 

Mambo hayo tunasoma katika Wafilipi sura ya pili mstari wa tano hadi wa kumi na moja.

5. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; 6. ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; 7. bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; 8. tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. 9. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; 10. ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; 11. na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba. (FIL 2:5-11)

 

Inaeleza kwanza kuhusu Yesu na jinsi alivyokuja hapa duniani kuokoa watu. Katika mstari  wa kumi, na wa kumi na moja, kuna jambo fulani zuri. Mungu atawakusanya watu wote hata wale watakaoingia Jehanamu na pia hata wale watakaokwenda Mbinguni. Pia malaika wote wa Mbinguni na wakuu wa malaika wote wa Mbinguni watakusanywa. Pia malaika wote ambao walioanguka na wale wakuu wa giza yaani wale wanaotawaliwa na Shetani. Na pepo wabaya pia watakusanywa.

 

Hawa wote watawekwa katika mistari mitatu mirefu. Kiti cha enzi cha Yesu kitawekwa katikati ya chumba. Mstari wa kwanza ni wa malaika wote wa Mbinguni. Mstari wa pili ni wa watu wote tangu Adamu. Mstari wa tatu ni wa Shetani na malaika wake wabaya na majeshi yake yote na pepo wabaya, yaani pepo wachafu.

 

Ninaomba niwe karibu na kiti cha enzi cha Yesu ili niweze kuona mambo yote tangu mwanzo. Matokeo hayo yatakuwa makubwa na ya ajabu ndio maana ningependa kuyaona. Sijui kama nitapata nafasi kuangalia mambo yatakayotokea huko.

 

Wote watakuja kuinama mbele za Yesu na kusema: YESU KRISTO NI BWANA! Kwa sababu malaika wa Mbinguni, watu wa dunia, na malaika wabaya wako wengi mambo haya pia yatachukua muda mrefu. Lakini huko hakuna upungufu wa muda.

 

Mstari  wa kumi, na wa kumi na moja, inaeleza juu ya mambo hayo. Ninayasoma tena: ... ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba. (FIL 2:10,11)

 

Biblia nyingine ya Kiswahili inasema: Ili kwa heshima ya jina la Yesu, viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu, vipige magoti mbele yake.

 

Na Biblia ya Kiswahili cha kisasa inasema: ... maana katika Jina lake Yesu wote wapige magoti, wao walioko mbinguni nao waliopo nchini nao walioko kuzimuni.

 

Kuna makundi matatu: walioko mbinguni, nao waliopo nchini nao walioko kuzimuni.

 

Tumesoma kwamba kwanza watakuja wale: walioko mbinguni.

Katika kundi hilo kuna malaika mamilioni. Hapo kuna maserafi na malaika wakuu. Mikaeli malaika mkuu wa Israeli atakuja. Atakuwepo Gabrieli malaika mkuu. Wao na malaika wengine watafika mbele ya kiti cha enzi cha Yesu.

 

Watapiga magoti na kusema: YESU KRISTO NI BWANA!

Labda malaika wa Mbinguni watasema hayo kwa heshima kubwa na shangwe. Halafu malaika wataondoka.

 

Kundi lingine litaingia.

Tumesoma, kwamba: kila goti lipigwe, .. wao nao waliopo nchini.

Yaani wanadamu wakiwa katika mstari watakwenda mbele ya Yesu na kupaza sauti: YESU

KRISTO NI BWANA! 

 

Katika kundi hilo kuna watakatifu, yaani sisi tuliookoka na kuvuka mto wa mauti. Sisi ambao damu ya Yesu imeisafisha mioyo yetu. Tutapiga magoti na kupaza sauti: YESU KRISTO NI BWANA!

 

Wengi watakuwa na nyuso zenye uheri. Sisi tumejifunza kupaza sauti hapa duniani wakati wa maisha yetu. Hata tumeweza kuirudia mara nyingi wakati wa maisha yetu.

 

Ningependa kuwa karibu na kiti cha enzi cha Yesu niweze kuangalia mambo hayo.

 

Wale watakatifu wa Agano la Kale pia watakuja. Huko watakuwepo Ibrahimu, Sara, Isaka na Yakobo. Mfalme Daudi pia atakuwepo, na wafalme wengine wa Agano la Kale. Manabii wa Agano la Kale pia watakuja. Hata Samweli, Isaya, Yeremia na Danieli watakuwepo.

Watakuja mbele ya Yesu na kupiga magoti na kusema: YESU KRISTO NI BWANA! 

 

Wanafunzi wa Yesu watakuja. Hata Yuda Iskarioti aliyemsaliti Yesu atakuja. Atakuja akiwa na uso wenye huzuni sana akizungusha vidole na kusema: Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia. (MT 27:4) Wafia dini waliokufa kwa ajili ya imani yao watakuja wakiwa na nyuso za furaha na heri. Watakuja na kupiga magoti mbele ya Yesu na kusema: YESU KRISTO NI BWANA!

 

Hata wewe uwe umeokoka au hujaokoka utapiga magoti mbele ya Yesu. Watakuja wale ambao wamepinga kwamba, "hakuna kuishi tena baada ya kifo, bali yote yatakoma baada ya kifo". Wao wamesema kwamba, hakuna Mungu, wala Yesu, wala Mbingu au Jehanamu.

 

Mmoja wao akiwa mwandishi wa vitabu wa Ufaransa alikuwa mwana falsafa Franqois Voltaire. Yeye aliishi mwaka wa 1694-1778, alikuwa maarufu wakati wake. Yeye alisema kwamba "baada ya miaka mia duniani hakutakuwepo na Biblia hata moja." Pia alisema kwamba baadaye watu hawatajali Biblia bali kumkana Mungu kutashamiri. Pia alisema kwamba jinsi maendeleo yanavyo ongezeka watu watakana dini.

 

Yeye alikosea. Miaka mia moja baada ya kifo chake chama fulani cha Biblia kilikuwa kimekodisha nyumba yake, na nyumba ile ikawa stoo ya Biblia. Yeye alisema kwamba baada ya miaka mia duniani hakutakuwepo na Biblia yo yote, lakini wakati huo nyumba yake ilijaa Biblia.

 

Yeye pia atakuja mbele ya Yesu kupiga magoti. Ningependa kwenda kwake na kumgonga mgongo wake na kusema: "Unaona kuna Mungu, Yesu na Mbingu na Jehanamu, - wewe ulipotoka."

 

Huko watakuwepo Hitler, Yaser Arafat, Saddam Hussein na Stalin na wengine wengi. Idi Amin atakuja. Wote watapiga magoti mbele ya Yesu na kupaza sauti: YESU KRISTO NI BWANA!

Hawapendi, lakini ni lazima. Hata waganga wa kienyeji watakuja. Waislamu wote watakuja. Hata wafuasi wa Buddha watakuja. Watapiga magoti mbele ya Yesu na kupaza sauti: YESU KRISTO NI BWANA!

 

Wengi watakuja mbele ya Yesu wakiwa na furaha na uheri usoni. Wao wamejifunza kushangilia maishani mwao na sasa wanashangilia mioyoni mwao. Wengine watakuja wakiwa na nyuso zenye huzuni. Wao walimkana Yesu maishani mwao. Wao walikataa kuokoka ingawa walihimizwa wafanye hivyo, yaani kuokoka. Mbele ya kiti cha enzi cha Yesu, ni lazima wamshangilie Yesu.

 

Halafu wanadamu wote wataondoka. Kila mmoja amekwisha paza sauti yake.

 

Tumesoma: kila goti lipigwe, (... wao walioko mbinguni nao waliopo nchini) nao walioko kuzimuni.

 

Mpaka sasa tumeangalia kama wao walioko mbinguni na nchini wamekuja mbele ya Yesu. Na sasa watakuja wale walioko kuzimuni, yaani malaika wa giza na mashetani wote.

 

Ningependa kuona mambo hayo nikiwa karibu na kiti cha enzi cha Yesu. Ni kweli kwamba ni mambo ya kusikitisha sana. Huko Shetani atatangulia, halafu wale waliokuwa wanatawala naye. Huko kuna malaika wabaya wa nchi mbali mbali. Hata malaika wale wa ubaya watakuja. Pia kundi kubwa la mashetani mbali mbali, yaani pepo wachafu. Pepo hawana mwili ndio maana wanawatafuta watu, ili waingie ndani yao wafanye kazi duniani. Wao hawana ruhusa kuingia ndani ya watakatifu wa Yesu bali wale tu waliojitoa kwa utawala huo. Yesu anaishi ndani ya walio wake. Mashetani yanaweza kutusumbua, lakini hayawezi kukaa pamoja na Yesu katika chumba kimoja. Lazima mmoja aondoke na yeye ni mnyonge, ni lazima mapepo yatoke, Yesu anapoingia na kuishi ndani ya moyo wa mtu.

 

Baada ya hukumu ya mwisho Shetani pamoja na malaika zake na mashetani wote watapiga magoti mbele ya Yesu. Kama nikipata nafasi ya kuona mambo hayo karibu na kiti cha enzi cha Yesu nitawaona wakipiga magoti na kupaza sauti: YESU KRISTO NI BWANA! Ndio lazima wapaze sauti. Wakiwepo Shetani, na majeshi yake wamenisumbua hata mimi sana. Ndio maana ningependa kuona wakati huo wakiwa wamepiga magoti mbele za Yesu. Itakuwa jambo la ajabu kuona jinsi gani shetani, utawala wake na malaika wote wabaya na pepo wachafu wamepiga magoti mbele ya Yesu.

Wao pia wanapaza sauti: YESU KRISTO NI BWANA!

 

Baada ya hayo wao watakwenda Jehanamu. Wao hawaendi huko peke yao bali wataenda pamoja, na wale ambao majina yao hayakuandikwa katika kitabu cha uzima. Yaani wale ambao hawajaokoka. Au kama mtu fulani aliokoka kisha akaacha wokovu yeye pia atakwenda katika hukumu ya milele. Baada ya malaika wote, watu wote na malaika wa shetani kupiga magoti mbele ya Yesu na kupaza sauti kuwa Yesu Kristo ni Bwana, - kila mmoja ataelekea sehemu yake.

 

Ni wakati huo sisi tutaingia ndani ya vyumba vya Mbinguni. Mng'aro wake ni wa ajabu. Huko tutavikwa taji. Ni taji ya ushindi. Labda tutaangalia kwa mshangao yale mazuri tutakayoona.

 

Tusome Ufunuo sura ya ishirini na moja mstari wa nne.

4. Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.  (UFU 21:4)

 

Huko hakuna kifo wala huzuni wala kilio. Magonjwa na maumivu yamebaki nyuma milele. Tumesoma kwamba: Naye atafuta kila chozi katika macho yao. Labda sasa mwingine anauliza: Je, huko kuna machozi? Je, machozi hayakubaki duniani? Ambapo machozi yalikuwa mengi sana? Je, hata Mbinguni kuna machozi?

 

Ninaelewa ni machozi ya furaha. Tutakapoingia Mbinguni na kugundua kwamba yote ya kale yamebaki nyuma labda tutalia kwa furaha. Pia tutalia kwa furaha kwa sababu tunajua kwamba hatutaanguka dhambini tena. Hakuna hatari kwamba, tutaacha wokovu, kama wakati ule tulipokuwa tunaenenda katika wokovu duniani. Wengi walianguka na hata sisi hatukuwa mbali. Lakini Mbinguni hakuna hatari hiyo. Labda ndio maana tutalia kwa furaha.

 

Halafu Mungu atakuja na kufuta hata machozi ya furaha katika macho yetu. Anasema: "Haya hayahitajiki hapa mbinguni. Hata machozi ya furaha ni ya ulimwenguni, hatuyahitaji hapa Mbinguni. Halafu atatufuta machozi katika macho yetu.

 

Labda wewe utasema huko Mbinguni: "Duniani kulikuwa na mateso na matatizo mengi." Na utaendelea kusema kama Paulo katika waraka wa Warumi: Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu. (RUM 8:18)

 

Na utaendelea kusema: "Ilikuwa vizuri kwa sababu niliokoka! Ilikuwa vizuri nilipobatizwa! Ubatizo ulinisaidia katika wokovu. Ilikuwa vizuri nilipotunza wokovu wala sikurudi nyuma! Ilikuwa vizuri nilipotoa mali zangu kwa ajili ya kazi ya Mungu! Ilikuwa vizuri nilipotumika katika kazi ya ufalme wa Mungu! Ilikuwa vizuri nilipoanguka nilitubu na kurudi tena! Sasa niko hapa Mbinguni milele."

Labda wengi watafikiri hivi huko Mbinguni.

 

Ninatumaini mimi na wewe pia tutakuwa huko pamoja na wengine. Natumaini hata jamaa zangu watakuwa huko. Ndio maana ninataka kuwaeleza watu mambo haya ili wengi waweze kukaa mbinguni milele na wala sio Jehanamu.

 

Nitakapoangalia taji yangu niliyopewa Mbinguni, labda nitamrudishia Yesu. Labda nitamwambia Yesu: "Mwenendo wangu, na kazi zangu duniani zilikuwa dhaifu wala sistahili kuibeba taji. Wakati mwingine nilichoshwa na wapendwa wako kwa sababu siku zingine walinisumbua. Hata wewe, Yesu nilichoka kukupenda kwani sikuweza kuelewa ni kwa jinsi gani ulivyonipitisha katika matatizo mbali mbali. Sikukumbuka kukushukuru kila mara bali nililalamika kuhusu hali yangu. Ndio maana sistahili kuibeba hii taji yangu. Chukua hii na umpe yule ambaye maisha yake ya wokovu yalikuwa mazuri zaidi."

 

Labda Yesu atasema: "Beba tu taji yako! Hapa mbinguni una wakati wa milele kujifunza neema ya Mungu ni nini." Na Yesu ataendelea: "Utajifunza juu ya yale yote niliyofanya kwa ajili yako." Ndipo Yesu atanijibu na kusema: "Hapa ndipo utaamini vizuri nguvu ya damu na ukubwa wa upatanisho. Taji hiyo siyo kwa ajili ya uzuri, au ukamilifu wako. Ni taji ya wenye dhambi waliosamehewa."

 

 

Sasa bado tuko duniani.

Sasa tupige mbio kuelekea umilele.

Sasa tunawaita watu waje katika wokovu na kuwatia moyo walio katika wokovu ili waendelee katika njia hii hadi mwisho.

Kila aliye wa Yesu, umilele mzuri unamsubiri.

 

 

Tutaonana Mbinguni!

 

 

----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------