Teuvo Kopra:
ZABURI YA WACHUNGAJI
Zaburi 23
1. Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. 2. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza. 3. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. 4. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya; kwa maana wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji. 5. Waandaa meza mbele yangu, machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, na kikombe changu kinafurika. 6. Hakika wema na fadhili zitanifuata siku zote za maisha yangu; nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (ZAB 23:1-6)
Tusome pia Petro wa kwanza sura ya tano na mstari wa kwanza hadi wa nne.
1. Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; 2. lichugeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. 3. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. 4. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka. (1PET 5:1-4)
Hapa tunaelezwa juu ya kazi yetu. Sisi ni wachungaji ndani ya kanisa la Mungu. Katika mstari wa nne tunaelezwa juu ya mchungaji mkuu. Yesu ni Mchungaji Mkuu nasi ni wasaidizi wake. Sisi ni wachungaji wa mshahara. Mshahara unatusubiri tukifika mbinguni. Kama tunatumikia kanisa vizuri tutapata mshahara mkubwa zaidi, lakini tukitumikia vibaya tunaweza kubaki bila ya mshahara.
Mchungaji Mkuu na wasaidizi wake wana kazi yao. Ni ujuzi wa Mungu kulinganisha kanisa na kundi la kondoo. Wakristo kanisani wanalinganishwa na kondoo. Ndani ya kundi la kondoo kuna mengi yanayofanana hata kanisani. Ndio maana kundi la kondoo ni mfano mzuri wa kanisa. Pia kondoo wana tabia sawa sawa zinazofanana na Wakristo. Ndio maana kondoo ni mfano mzuri wa washirika wa kanisa.
Kondoo wanataka wawe pamoja kama Wakristo kanisani. Kondoo wanamfuata mchungaji kama Wakristo ndani ya kanisa. Yesu anatangulia nasi tunamfuata. Na pia Wakristo wanawafuata wachungaji wa kanisa. Ndio maana ni muhimu sana kuangalia jinsi sisi wachungaji tunavyoishi na kuenenda. Tunapochunga kanisa la Mungu ni vizuri kukumbuka kwamba mwenye kundi ni Yesu mwenyewe. Sisi ni wasaidizi. Kundi siyo letu. Kanisa siyo letu. Kanisa ni la Mchungaji Mkuu, yaani la Yesu Kristo. Sisi tunachunga kondoo lakini kondoo siyo mali yetu. Ni muhimu sana kukumbuka hayo.
Kuna kondoo mbali mbali ndani ya kundi. Na pia ndani ya kanisa kuna Wakristo tofauti tofauti. Nasi tunapaswa kuwachunga wote. Hatuwezi kuwabadilisha wote wafanane. Mchungaji Mkuu ametuumba tofauti tofauti. Anataka tukubali kwamba sisi watu ni tofauti tofauti. Mchungaji Mkuu anakubali hayo nasi tunapaswa tuyakubali pia. Ndani ya kondoo wa duniani kuna wengine wanono. Wanakula chakula kingi. Hata kanisani kuna watu wanene sana kiroho. Yaani wanakula chakula kizuri cha kiroho ndio maana ni wanene.
Pia kondoo wa duniani kuna kondoo wengine waliokonda. Labda ni wagonjwa au hawali wakashiba. Kanisani kuna wengine ambao wamekonda kiroho. Inawezekana hawaendi kanisani mara kwa mara. Au hawasomi Biblia na hivi hawapati chakula cha kiroho. Kwa maana hiyo wamekonda kiroho. Labda wengine kanisani ni wagonjwa kiroho. Ndani ya kundi la kondoo kuna kondoo wengine wenye mimba. Ndio maana mchungaji anawatembeza taratibu ili baadaye kondoo waweze kuzaa watoto wenye afya.
Mara kwa mara mchungaji anachunguza kundi la kuchunga ili hali ya kondoo ingekuwa nzuri. Yeye hawapeleki haraka wala pole pole sana. Ni sawa hata ndani ya kanisa. Ni lazima tuchunguze Wakristo kanisani. Na kuwaongoza kwa njia inayofaa, ili Wakristo wajisikie vizuri.
Iwapo Wakristo wanaendelea vizuri wanaweza kuendelea kuzaa kondoo wengine wapya. Hali ya kiroho ikiwa nzuri kanisani inakuwa vizuri zaidi. Wakipata chakula kizuri cha kiroho wana afya nzuri kiroho pia. Ni muhimu kutoa chakula kizuri cha kiroho na chenye afya njema.
Pia kuna kondoo wengine ndani ya kundi wanao gonga wenzao. Na wanasababisha matatizo mara kwa mara kwa mchungaji. Pia kanisani kuna wale wanao pigana na kugombana na wenzao. Hao wanaleta matatizo kwa wachungaji kanisani lakini tukumbuke kwamba hao pia ni wapenzi wa Mchungaji Mkuu, yaani Yesu Kristo. Tuwapende na hao pia ingawa si kazi rahisi.
Ndani ya kundi la kondoo kuna wengine wagonjwa. Wengine hawatembei vizuri, wanatembea kwa kuchechemea. Ndani ya kanisa kuna pia wengine ambao hawajakuwa vizuri kiafya. Wengine wanaendelea kuchechemea. Wengine wanaanguka zaidi ya wengine. Mara nyingine inatulazimu kuwabeba wengine. Hawa wanatuletea matatizo. Tunahuzunika na mienendo yao.
Ni lazima tukumbuke kwamba kanisa siyo letu. Wakristo sio wetu bali wa Yesu. Lazima tuenende nao kama vile Yesu Kristo anavyoenenda na sisi. Yeye ni Mchungaji Mkuu sisi ni wasaidizi wake. Tunapaswa kuuliza matakwa yake ili tuweze kuvumiliana na hao Wakristo wenye matatizo.
Ndani ya kundi la kondoo kuna wengine wazee na wengine vijana. Ndivyo ilivyo ndani ya kanisa. Kondoo wanatofautiana katika tabia. Wengine wana upungufu katika tabia. Ndivyo ilivyo hata kanisani. Mara nyingine tunaweza kushangaa kwa nini Wakristo wanaenenda hivyo. Au tunashangaa kwa nini wanaongea hivyo. Wanatofautiana. Mungu ametuumba tofauti tofauti. Tusijaribu kuwabadilisha wafanane kwani Mungu amewaumba kwa hali hiyo.
Mchungaji wa kondoo ana kazi kidogo sana pamoja na kondoo wanaotii na wazuri. Lakini wale wenye matatizo wanaleta na wanasababisha matatizo mengi kwa wachungaji. Ndani ya kanisa wengine wanawasababishia wachungaji matatizo mengi na wengine matatizo madogo madogo tu. Muda mwingi mchungaji anawahudumia wale kondoo wenye matatizo. Ni sawa hata kanisani wachungaji muda mwingi wanajaribu kuwasaidia wale ambao wana matatizo na wanaogombana na Wakristo wengine na watu wengine.
Ndio maana wachungaji wanapata ndani yao picha isiyo sahihi na ya kukanusha kundi kwa maana wanafanya kazi kati ya matatizo mengi. Ndio maana sisi wachungaji tunahitaji maombi mengi na kusoma Biblia kwa bidii ili tuone kanisa kwa macho ya Mungu. Tukiangalia kanisa na Wakristo kwa macho ya mwilini tunaona tofauti na kama vile tungewaangalia kwa macho ya Mchungaji Mkuu Yesu Kristo.
Akiwepo mgonjwa katika kondoo wakufugwa mchungaji anamchinja. Hivyo anapata kundi la hali ya juu. Hapo wanao kondoo wazuri na wenye afya tu. Sisi tukiwa wachungaji katika kundi la kondoo wa Yesu kanisani, tunapaswa kufanya yale anayotaka Mchungaji Mkuu. Mchungaji Mkuu wetu hajaturuhusu kuchinja hata kama kuna mgonjwa au mwenye hitilafu na aliye konda. Haturuhusiwi kuchinja hata yule anayowapa kondoo wenzake matatizo mara kwa mara, Wakristo wengine kanisani. Hata wale wanaotupiga na kutugonga gonga. Kuchinja ni sawa na kama kutenga Mkristo fulani ambaye amekwisha kuokoka. Au tunakataa atafika mkutanoni. Au tunakataa ushirikiano na Wakristo wengine.
Lakini fulani akipoteza hali yake ya kiroho na asitubu baadaye huyo amekufa kiroho. Huyo aliyekufa kiroho ni lazima atengwe lakini siyo yule Mkristo dhaifu kama ana uhai wa kiroho. Kondoo hawa wa kawaida akifa katika kundi anatolewa. Hata wale wanao eneza magonjwa ya kuambukiza. Ni sawa ndani ya kanisa la kiroho: walio rudi nyuma au walio kufa kiroho na hawataki kutubu ni lazima watengwe. Hata ambao kukaa kwao kanisani wanachafua sana kanisa. Kutenga kufanyike kwa njia nzuri ili hata baadaye aweze kwa urahisi kurudi kanisani.
Wakati wa Agano la Kale waliofanya kazi ya kiroho waliitwa makuhani. Kama fulani alifanya dhambi alienda hekaluni kwa kuhani. Alikuwa na kondoo kwa ajili ya dhabihu. Mwenye dhambi aliungama dhambi zake mbele ya kuhani na kondoo alichinjwa kwa ajili ya dhambi zake. Hivyo mwenye dhambi alisamehewa. Huu ni mfano wa kazi ya dhabihu aliyofanya Yesu alipokufa msalabani kwa ajili yetu. Kuhani aliwatumikia wenye dhambi katika eneo la hekalu. Kuhani alisikiliza maungamo ya dhambi na alisaidia katika kuchinja. Yaani kuhani alikuwa mchinjaji. Mtu alipofanya dhambi kuhani alichinja kondoo. Hayo yalifanyika wakati wa Agano la Kale.
Katika Agano Jipya sisi siyo makuhani yaani wachinjaji bali wachungaji. Haturuhusiwi kuchinja kondoo kwa sababu ya dhambi Yesu alikwisha chinjwa kwa ajili ya wenye dhambi. Bali kama kondoo fulani yaani aliyeokoka akaanguka dhambini ni kazi yetu kumsaidia ili apate msamaha. Hatumtengi bali tunajaribu kumtibu. Mchungaji wetu Mkuu hajatupa ruhusa ya kuchinja bali ametuamuru kulisha na kuchunga kondoo. Sisi ni wachungaji ndani ya kundi la kondoo wa Yesu.
Ndani ya kundi la kondoo kuna kondoo tofauti. Tunapowachunga mara nyingine tunawashangaa. Au hata tunaweza kukasirikia mmoja wao. Mara zingine tunashangaa sana na matendo ya wengine ndani ya kundi usemi wake wa matendo yake. Tunataka wote katika kundi letu wawe wazuri na wawe na tabia njema. Ndio maana wakati mwingine tunatumia hasira au tunatoa fimbo. Na fulani akiwa ameshindikana tunataka tumpeleke machinjioni yaani kutenga kanisani. Ndio ni lazima tuwe na adabu kanisani lakini tunaweze kuwa wakali kupita kiasi.
Kutokuwa na utii ni jambo mbaya kanisani. Katikati ya matatizo hayo tunapaswa kukumbuka kwamba kundi siyo letu. Kondoo siyo wetu. Sisi ni wachungaji wa kundi la kondoo wa mgeni. Mwenye kundi yaani Yesu anatuambia wachungaji: "Ni kundi langu. Kondoo ni kondoo wangu. Mimi nimekuwa uwe mchungaji si mchinjaji." Mwenye kondoo anaendelea kusema: "Unisaidie kuwasafirisha kundi la kondoo hadi nyumbani." Ni kazi yetu kuwasafirisha kundi la Yesu ili siku moja wafike mbinguni.
Tulisoma Zaburi ya ishirini na tatu. Inaeleza juu ya mwenendo wa kondoo mmoja, yaani mwenendo na maisha ya aliyeokoka. Ujumbe wa Zaburi hii unaanza kwa maisha ya mwanzoni wa aliyeokoka na kuendelea katika maisha ya wokovu hadi mwisho.
Tulisoma kwanzia mstari wa kwanza. Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. (ZAB 23:1) Mchungaji Mkuu anataka kuwapeleka kondoo wote yaani waliookoka katika hali hii. Lakini kwa sababu Yesu hayuko nasi kimwili anatutumia sisi. Yeye ametupa sisi wasaidizi wake kazi ya uchungaji.
Katika Zaburi hii anatueleza jinsi sisi tunavyopaswa kuchunga kondoo yaani Wakristo ndani ya kanisa. Aliyeokoka karibuni anapaswa kujua kwamba amepata hazina nzuri sana. Pia afundishwe na ajue kwamba Yesu ni mchungaji wake na siyo wazee au wahubiri. Sisi ni wasaidizi tu.
Anapaswa kujua kwamba amepata utajiri mkubwa katika maisha yake, amepata wokovu moyoni mwake. Ingawa atapungukiwa na vitu vingine vya duniani lakini amepata hazina kubwa na utajiri wote wa duniani ni takataka mbele yake. Yeye amesamehewa dhambi zake na anasafiri kwenda mbinguni.
Tulisoma mstari wa pili kwamba: Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza. (Zab 23:2) Kondoo anaweza kula chakula kizuri. Kondoo siyo mnyama wa mapambano kama simba. Kondoo siyo mnyama wa kazi kama punda au fahali. Kazi ya kondoo ni kula, kupumzika na kuzaa kondoo wengine. Ndio maana ni muhimu aliyeokoka apate chakula kizuri cha kiroho na apumzike.
Waliokoka wengi wana njaa ya kiroho. Tuwape chakula. Ni kazi ya mchungaji kuwapeleka kwenye malisho mazuri. Pia tulisoma kando ya maji ya utulivu huniongoza. Biblia inatumia mifano mingi. Tumeona kwamba kanisa linafananishwa na kundi la kondoo. Mkristo anafananishwa na kondoo. Na pia maji ina mifano mingi. Biblia neno la Mungu ni kama maji. Baraka ni kama maji. Ujazo wa Roho Mtakatifu ni kama maji.
Tunapomwongoza aliyeokoka kando ya maji ina maana kwamba tunamwelekeza katika kusoma neno la Mungu. Na pia kupokea baraka mbali mbali za kiroho. Ni muhimu sana ajazwe na Roho Mtakatifu. Mchungaji Mkuu ametuweka tuwe wasaidizi wake ili malengo yake juu ya aliyeokoka yatimia. Maji na chakula ni muhimu kwa kondoo. Bila ya hayo kondoo anadhoofika na hatimaye kufa. Ni sawa kwa Wakristo chakula cha kiroho na baraka za rohoni ni muhimu. Bila hayo wanapoteza maisha yao ya kiroho na labda hawatafika siku moja mbinguni.
Watu wakiwa na njaa wanakuwa wakali na wanagombana hata kwa kitu kidogo. Kama kanisani kuna njaa ya kiroho wana gombana mara kwa mara. Nimekuwa mchungaji ndani ya makanisa ambapo ugomvi umesababisha makanisa kuharibika. Nimeenda kwenye kanisa iliyobomoka na nimehubiri neno la Mungu. Ni kama mkate yenye uhai. Wao wamekula chakula cha kiroho na kupokea baraka za rohoni wao wamepata nguvu na afya. Makanisa yamepata uvuvio. Wakristo wamerudi tena kanisani.
Kama ningalijaribu kuwachapa ili warudi nisingalifaulu. Kanisa ambao limepata fimbo linazidi kuharibika. Bali nimewaleta pamoja kwa neno la Mungu, kwa chakula kiroho. Chakula kinawaunganisha watu, wanakuja kwa sababu wanaweza kula chakula kizuri. Wakristo wasipopata chakula cha kiroho wanaenda kutafuta chakula katika makanisa mengine au mahali pengine. Kule wanaweza kupata chakula chenye sumu inayoweza kuharibu maisha yao ya kiroho. Kazi ya mchungaji ni kuwapeleka kundi katika malisho mazuri waweze kula na kupumzika.
Pia wanywe maji masafi. Kondoo hajui kutafuta mwenyewe ndio maana anahitaji mchungaji. Ni sawa hata kwetu kanisani. Wachungaji wana kazi kubwa muhimu. Tupate wapi maji masafi? Yaani tupate wapi chemchemi za baraka kwa Wakristo ili iwe faida kwao hata milele? Ndani ya chemchemi kuna maji. Biblia inaeleza juu ya chemchemi mbali mbali za baraka na tunataka kuwaelekeza Wakristo huko. Wanapo kunywa kwenye chemchemi hizo wanapata baraka.
Maana kwako Wewe iko chemchemi ya uzima, katika nuru yako tutaona nuru. (ZAB 36:9)
Yaani tunapowaongoza waliookoka karibu na Mungu wataweza kunywa ndani ya chemchemi za baraka. Pia wanaona nuru wanapokaa karibu na Mungu.
Kinywa chake mwenye haki ni chemchemi ya uzima; bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu, (MIT 10:11)
Tunapozungumza na watu vinywa vyetu vinapaswa kuwa chemchemi ya uzima. Wakristo wanataka kuzungumza na wachungaji kwa sababu wanataka kupata burudisho la kiroho.
Sheria ya mwenye akili ni chemchemi ya uzima, ili kuepukana na tanzi za mauti. (MIT 13:14)
Tunapofundisha kanisani Mchungaji wetu Mkuu anataka mafundisho yetu yawe kama chemchemi ya uzima. Hiyo ikiwepo Wakristo wanapata kunywa maji masafi.
Kumcha Bwana ni chemchemi ya uzima, ili kuepukana na tanzi za mauti. (MIT 14:27)
Tunataka kuwaongoza watu katika kumheshimu na kumcha Mungu. Hiyo ni baraka kwao ni kama kondoo wanapokunywa maji mazuri.
Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwake aliye nao; bali kufundishwa kwa wapumbavu ni upuzi wao. (MIT 16:22)
Wakristo wanapopata ufahamu wa wokovu zaidi hiyo ni chemchemi ya uzima kwao. Ndio maana Mungu ametuchagua katika kazi ya uchungaji ili kupitia sisi aweze kulisha kundi lake, kanisa lake. Pole pole kondoo anakuwa na kupata nguvu.
Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya. (EBR 5:14)
Hii inatokea taratibu. Hivyo kazi yetu katikati ya Wakristo inapungua. Lakini tu kama yeye amekuwa vizuri kiroho. Ni hivyo kama tutawalisha vizuri na watakua baadaye tutapata kazi rahisi zaidi.
Lakini tukifanya kazi yetu vibaya Wakristo watabaki kuwa watoto siku zote. Wao hawajakuwa kiroho bali wao wanakuwa watoto wa kiroho. Tulisoma Zaburi ishirini na tatu, mstari wa tatu: Hunihuisha nafsi yangu; (Ps 23:3a) Mchungaji Mkuu anataka kuhuisha roho za Wakristo. Kabla ya wokovu roho ilikuwa imenyauka sasa inahuishwa. Hii ni nia ya Mchungaji Mkuu, nasi tuwe hivyo.
... na kuniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. 4. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya; kwa maana wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (Ps 23:3b, 4)
Mchungaji anataka kuwaelekeza njia sahihi. Yesu pia anataka walio wake wafuate katika nyayo zake. Njia yake mara nyingine sio rahisi kwetu. Hatuelewi ni kwa nini anaongoza maisha yetu anavyoongoza. Njia zingine zingekuwa rahisi zaidi. Mstari wa tatu inaeleza juu ya kuongozwa katika njia ya haki.
Mstari wa nne inaeleza juu ya bonde la mauti. Biblia zingine mpya zaidi inaeleza kwamba: ...bonde la giza kuu. Yaani Yesu anawaongoza walio wake katika bonde la mauti, bonde la giza kuu. Ninaelewa hapa kwamba inatueleza juu ya mambo magumu na majaribu makubwa. Hayo yanapatikana ndani ya maisha ya kila mmoja wetu. Wakristo wengine wanaenenda ndani ya majaribu makubwa. Wana magonjwa, umasikini na mambo mengine magumu. Pia kuna vita na kifo. Hatujui ni kwa nini tunapelekwa huko.
Watu wanafikiri mtu akiteseka sana ni kwa sababu yeye ni mwenye dhambi sana. Watu wanafikiri kwamba matatizo na ajali kubwa zinatokana na dhambi. Watu wanasema: Ukipata matatizo au ajali kubwa ni kwa ajili ya dhambi. Siyo kweli. Biblia inasema wafuasi wa Yesu wana matatizo mengi. Matatizo siyo adhabu bali yanahusu maisha ya watu wote, pia Wakristo.
Wakristo wachache sasa hivi wanatembea ndani ya bonde la uvuli wa mauti. Wana magumu makubwa. Katikati ya mambo hayo Yesu anataka kuwaongoza na kusaidia. Yesu anahitaji wachungaji wasaidizi waweze kuwasaidia walio katika magumu mbali mbali. Kama kanisani mchungaji yuko karibu nao na anawaelewa wanakuwa na hali rahisi zaidi. Hawachoki katikati ya matatizo yao makubwa kama mchungaji yuko karibu nao. Ndio maana unahitajiwa.
Hata sisi wachungaji tunatembea katikati ya bonde la uvuli. Hata sisi tunajaribiwa kwa matatizo mbali mbali. Bwana wetu anataka tuweze kuzoea bonde hilo la matatizo. Tukiwa tumepazoe tunaweza kuwasaidia wale ambao wako huko hivi sasa. Na kwa sababu tumepazoe hatupotei huko. Tunaweza kuwaongoza wale Wakristo ambao wanatangatanga huko. Kwa sababu Yesu anataka tufahamu bonde la uvuli vizuri anatupeleka huko mara kwa mara. Hata huko kuna njia ambayo tunaweza kupita.
Tulisoma pia: sitaogopa mabaya; kwa maana wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (Ps 23:3b, 4)
Watu wanaogopa katika matatizo yao. Yesu anataka awe pamoja na watu wakati wa majaribu. Lakini anatutumia sisi twende na watu hawa. Hawahitaji kuogopa kwa sababu mchungaji anatembea karibu nao.
Gongo na fimbo hayo hayatumiki kwa kuchapa kondoo bali ni kwa ajili ya adui. Kondoo anagundua kwamba mchungaji anamtetea. Hata sisi tunatakiwa tuwatetee wale walio katika matatizo, si kuwalaumu kwamba ni kwa ajili ya mwenendo wao mbaya ndio maana wamepotea. Mara nyingi majaribu yanakuja kwa mwongozo wa Mchungaji Mkuu. Wengine wanauliza bonde la uvuli lina faida gani? Lina faida nyingi. Ndio maana Yesu anatupeleka huko. Huko tunaweza kumjua Yesu vizuri. Tunaomba zaidi. Tunakuwa wanyenyekevu. Tunawahurumia wale walio dhaifu.
Waandaa meza mbele yangu, machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, na kikombe changu kinafurika. (ZAB 23:5)
Eti bonde hilo haliendelei hata milele. Siku zingine tuna majaribu, wakati mwingine ni rahisi zaidi. Mambo ya mstari huu yanafanyika baada ya bonde la mauti. Na yanayofanana na hayo tuliyapata kabla ya bonde la mauti.
Tulisoma: Waandaa meza mbele yangu. Yaani Mchungaji Mkuu anataka kulisha kondoo wake. Tena anatumia wasaidizi yaani sisi. Kabla ya bonde la giza ya mauti kondoo alilazwa kwenye majani na kula chakula kibichi. Wakati wa majaribu hawezi kula vizuri lakini baada ya majaribu ataweza tena kula chakula cha kiroho.
Tulisoma: Waandaa meza mbele yangu, machoni pa watesi wangu. Tuna watesi wengi wanaotupinga. Shetani ni mtesi mkubwa. Dhambi mbali mbali zinatatiza maisha yetu ya wokovu. Pia sisi tuna mwili wa dhambi unaotaka dhambini. Ingawa tuna maadui na watesi wengi tunaweza bado kula chakula cha kiroho.
Kumfuata Yesu hakuondoi majaribu. Matatizo pia hayaondoi majaribu. Lakini katikati ya hayo yote tunaweza kula chakula cha kiroho. Ni lazima wachungaji wajue hayo. Ndio maana wanajifunza hayo mara kadhaa.
Pia tulisoma: Umenipaka mafuta kichwani pangu.
Agano la Kale inaeleza juu ya kupakwa mafuta. Watu walipakwa mafuta kwa ajili ya kazi fulani, mfano mfalme. Au alipakwa kwa ajili ya kazi fulani kama nabii. Mungu anakuza Wakristo kwa ajili ya kazi fulani. Kama wachungaji tunawasaidia wakue. Hasa wale ambao wamepita katika shule ya majaribu mbali mbali ni watumishi wazuri.
Tulisoma pia: na kikombe changu kinafurika. (Zab 23:5b)
Mungu anataka kuwabariki wale ambao anaweza kuwatumia. Tunawaongoza na kuwasaidia Wakristo kanisani ili Mungu aweze kuwatumia zaidi. Tutumaini ili Mungu aweze kuwatumia wao zaidi ya sisi. Hatuna wivu hata kama Mungu anawatumia Wakristo zaidi yetu. Tunaogopa kwamba Wakristo wengine wanaweza kurudi nyuma. Lakini kama wengine wamejaribiwa na wamesimama wao wana nguvu zaidi. Hatuwezi kuogopa kwa ajili ya wokovu wa kondoo huyu. Kondoo walio kuwa wanapaswa kupewa kazi kulingana na umri wao.
Hakika wema na fadhili zitanifuata siku zote za maisha yangu; nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (Zab 23:6)
Yesu anataka Wakristo waweze kuona maisha ya wokovu kwa njia hii. Sio tu wakati wa baraka bali kila siku. Hata wakati wa majaribu waona uzuri wa Mungu. Kuwaambia tu hivyo haitoshi. Bali waweze kuelewa hayo hata katika wakati mgumu. Pia wajue kwamba Mungu ni mwema.
Tukihubiri juu ya Mungu mkali watamwelewa Mungu kwa njia isiyo sahihi ndani ya mioyo yao. Tukihubiri juu ya Mungu wa upendo wao wanaona Mungu mwema. Hivyo tunapaswa mara nyingi kuhubiri juu ya upatanisho. Pia tuelekeze mawazo ya wasikilizaji juu ya dhabihu ya Golgotha. Huko Mungu anaonyesha upendo wake juu yetu ya wenye dhambi. Hubiri mara nyingi juu ya upatanisho na damu ya Yesu. Hivyo Wakristo wanajua Mungu ni mzuri na mwema.
Jambo la mwisho Daudi, mwandishi wa Zaburi anaandika kwamba anafurahi kukaa ndani ya nyumba ya Mungu milele. Hiyo sio lazima bali hiari hivyo tunaweza kumshukuru Mungu.
Marudio: Kwanza kondoo alifurahia malisho, maji ya utulivu kupumzika na uhuisho wa rohoni. Tena baada ya majaribu alifurahi kuweza kukaa ndani ya nyumba ya Mungu yaani kanisani. Sasa sio muhimu kwamba anapata nini katika wokovu bali kwamba anaweza kuabudu wapi au kukaa wapi.
Kondoo wanatofautiana sana. Ni sawa hata kanisani kuna Wakristo tofauti tofauti. Wao wanaona wokovu kwa njia tofauti. Mwingine anahuishwa nafsi na mwingine anashtuka kuingia ndani ya bonde la giza. Wakati huo Mkristo anakula katika malisho mabichi na kunywa maji ya utulivu lakini mwingine ambaye alikuwa katika majaribu anafurahi anapopata kula ingawa ana majaribu.
Ni lazima mchungaji pia apate kula. Ni muhimu ili mchungaji pia apate chakula. Wakati mwingine mchungaji anapata njaa wakati analisha kondoo. Au mchungaji ana kiu ingawa anawanywesha wengine maji masafi ya baraka. Chakula cha mchungaji na kula kwake ni tofauti na kondoo. Wakristo wanapata chakula cha kiroho na baraka za rohoni kanisani na mkutanoni.
Lakini wachungaji hawazipati mikutanoni kama watu wengine. Wachungaji sehemu yao ya chakula ni tofauti. Wao wanajitayarishia mara nyingi chakula chao. Yaani wachunguze zaidi ndani ya neno la Mungu. Wao wanatakiwa wapate wenyewe chakula ndani ya maombi. Haitosi tu wanapoenda mkutanoni.
Ni muhimu tukumbuke kwamba watu wote wanapendwa na Mchungaji Mkuu, Yesu Kristo. Nasi pia tuwapende. Kwa sababu alikuchagua ili aweze kufikisha kundi lake ndio maana alikuchagua uwe mchungaji. Kwa msaada wako anataka kuwa fikisha kundi lake nyumbani.
Biblia inasema: Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; (EFE 5:25b)
Upendo wake alionyesha Golgotha. Yeye anachunguza namna gani tunaenenda na kondoo wake. Tuulize: Unataka tulishe kondoo wako namna gani na kuwaongoza. Tunasubiri siku moja tuweze kuliongoza kundi hili dogo mbele ya Mchungaji Mkuu. Na natumaini tunaweza kusema: Hakuna aliye baki, wote ni salama.
Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichugeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka. (1PET 5:1-4)
Mungu akubarikie sana na kazi yako!